Poland imetangaza siku saba za maombolezi kufuatia kifo cha Rais Lech Kaczynski na maafisa wengine waandamizi wa serikali katika ajali ya ndege, magharibi mwa Urusi. Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, alisema hili ni janga kubwa kuwahi kutokea nchini humo katika historia ya siku za hivi karibuni.
Maelfu ya watu, wengi wao wakitokwa na machozi, waliizingira ikulu katika mji mkuu,Warsaw,wakiweka mashada ya maua na mishumaa.Waziri Mkuu wa Urusi, Vladimir Putin, amesema atasimamia uchunguzi kuhusu ajali hiyo ya ndege, karibu na mji wa Smolensk, ambapo miongoni mwa waliouwawa ni mke wa Rais Kaczynski, na viongozi wengine kadhaa waandamizi wa kijeshi na wa kiraia kutoka Poland.
Putin alizuru eneo la ajali akiambatana na Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk.
Waongozaji wa safari za ndege wa Urusi walisema rubani wa ndege hiyo alijaribu kutua wakati kukiwa na ukungu mkubwa, akipuuza ushauri aliopatiwa wa kuielekeza ndege hiyo kwingineko kutokana na hali hiyo mbaya ya hewa.
Ujumbe wa Poland ulio-ongozwa na hayati Rais Kaczynski ulikuwa na lengo la kuhudhuria maadhimisho ya miaka sabini tangu kutokea kwa mauaji ya halaiki katika mji wa Katyn, ambapo maelfu ya maafisa wa Poland waliuwawa. Maafisa hao wa Poland waliuwawa na polisi maalum wa iliyokuwa Muungano wa Kisovieti wakati wa vita vya pili duniani.