Wednesday, April 14, 2010

WACHIMBAJI 8 WAFA MGODINI GEITA

Kamanda wa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Ghasia (FFU), Mkoa wa Mwanza(aliyenyoosha kirungu), ambaye jina lake halikupatikana akitoa amri ya kuwaondoa wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Sobora wilayani Geita ili wasiendelee kuchimba baada ya wenzao 16 kuhofiwa kufa.(Picha na David Azaria).

Vilio na simanzi vimetawala katika maeneo kadhaa wilayani Geita baada ya wachimbaji wadogo 16 kuhofiwa kufa na wengine zaidi 20 kujeruhiwa baada ya kufukiwa ndani ya mgodi wa dhahabu.

Ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Sobora kata ya Kaseme, Butundwe, ambapo inadaiwa zaidi ya wachimbaji 60 walifukiwa na kifusi katika moja ya mashimo makubwa ya mgodi huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Simon Siro, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tayari maiti wanane wametambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya maziko.

Kamanda Simon alithibitisha kwa mwandishi wetu, kwamba hadi jana watu wote walikuwa wameondolewa ndani ya mgodi na hakuna mtu au maiti iliyesalia ndani.

Hata hivyo habari zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilieleza kwamba maiti 15 waliopolewa jana na kila aliyetambuliwa na ndugu au jamaa alichukuliwa na kusafirishwa kutoka eneo la tukio kwa ajili ya maziko.

“Tuliokuwa ndani ni zaidi ya 60 kwa sababu baada ya kubaini kwamba kuna dhahabu nyingi, tuliingia kwa wingi na kila mmoja alikuwa akichimbua dhahabu na ghafla kifusi kikatuangukia na kutufukia, kwa bahati nzuri mimi ni miongoni mwa watu walionusurika,” alisema mmoja wa manusura, Masanja Jamatoni (28) mkazi wa Katoro.

Aliongeza, kwamba hadi jioni maiti 16 waliopolewa kutoka shimo hilo, lakini katika hali ya kushangaza, kila baada ya maiti kuopolewa, watu walikuwa wakichanga fedha na kuwapa ndugu, jamaa na marafiki ili kusafirisha maiti huku wengine wakiendelea na uchimbaji.

Taarifa zaidi kutoka kwa baadhi ya wachimbaji wa eneo hilo, zilieleza kwamba kuna maiti waliosafirishwa kwenda kijiji cha Masumbwe, Shinyanga; Nyarugusu, Geita na wengine Matabe, Biharamulo mkoani Kagera ambao Polisi mkoani hapa ilishindwa kuwathibitisha.

Majeruhi mwingine, Masingija Maduhu (38) wa kijiji cha Nyarugusu alisema sababu kubwa ya kila maiti aliyeopolewa kusafirishwa kutoka eneo la tukio ni kuondoa usumbufu unaoweza kujitokeza kwa kuzuiwa kuendelea kuchimba katika eneo hilo.

“Si unaona, kama sasa hivi tayari tumepigwa marufuku kuchimba katika eneo hili kwa muda … haya ndiyo miongoni mwa mambo ambayo yalikuwa yanasababisha jana kila maiti anayeopolewa asafirishwe haraka kwenda kwao baada ya kutambuliwa, ili watu waendelee na uchimbaji,” alidai Maduhu.

Maiti waliotambuliwa hadi jana mchana ni Lugembe Nagogo (37) na Peter Malugu wakazi wa Bunda, Mara na Mirumbe Chacha (38) wa Musoma Vijijini, ambao hadi mwandishi wa habari hizi anaondoka eneo la tukio walikuwa ndani ya magari tayari kusafirishwa kwenda Mara.

Wengine waliotambuliwa ni David Marwa wa Katoro ambaye maziko yake yalifanyika jana mchana baada ya uchunguzi wa daktari kufanyika; wengine waliotambuliwa kwa jina moja ni Juma, John na Sumbu, wa kijiji cha Lwamgasa, ambao walisafirishwa kwenda Lwamgasa kwa ajili ya maziko.

Majeruhi waliolazwa wodi namba nane ya hospitali ya wilaya mjini hapa ni Masumbuko Magene (26) wa Nyarugusu, Mabula Mbeshi (33) wa Lwamgasa ambaye amevunjika miguu na kiuno na Sumbu Magembe.

Wengine ni Amos Samwel, Paul Nyamhanga, Mapambano Manyanda, na Shisho Musa na Lawrent Lutobeko (29) wote wa Katoro.

Habari zaidi zilidai kuwa zaidi ya wachimbaji wadogo 30 walinusurika baada ya kuopolewa wakiwa hai.

“Kilichotusaidia ni kwamba hapa kuna dhahabu nyingi kwa hiyo baada ya kufukiwa, wachimbaji waliokuwa nje walifanya kazi kubwa ya kufukua na kututoa ili waendelee kuchimba dhahabu, kwa sababu walikuwa wakitufukua huku wao wakiendelea na uchimbaji na cha ajabu kuna baadhi yetu baada ya kuopolewa, waliendelea tena kuchimba,” alisema Masumbuko Mageme aliyelazwa.

Ofisa Madini Mkazi wa Kanda ya Geita, Donald Mremi, alitoa tangazo la kusitisha uchimbaji dhahabu katika mgodi huo kwa muda, agizo ambalo lilitekelezwa na askari Polisi waliokuwa wakiongozwa na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Wilaya ya Geita, Paul Kihimbila kwa kuwaondoa wachimbaji hao eneo hilo.

Alisema kwamba mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya IAMGOLD.