Saturday, April 10, 2010

JK AWAONYA VIONGOZI CCM

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakaobainika kutoa kinyemela kadi za chama hicho watakiona.

Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ametoa onyo hilo wakati alipozungumza katika warsha ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na wenyeviti na makatibu wa wilaya wa CCM.

Kikwete amesema, tabia ya baadhi ya viongozi hao imesababisha watu wasiostahili kupata kadi hizo bila kutambuliwa.

Kikwete amesema, kadi zitakuwa zikitolewa kwa watu wanaoikubali na kuitii Katiba ya CCM.

"Katiba ya chama ina kanuni zake za wazi, mwenye sifa ndiye anayestahili … zisitolewe kinyemela, kwani kwa kufanya hivyo mtasababisha mgawanyo ndani ya chama," alisema Kikwete jana.

Kama mtu atahitaji kujiunga uanachama hana budi afuate utaratibu uliopo. Alisema ni matarajio yake kuwa CCM haina mgawanyiko. Aliwasisitiza pia wanachama kulipia ada kadi zao na kujiandikisha katika madaftari ya wanachama ili wajulikane pia idadi yao.

Kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu, alisema CCM imejipanga kupata viongozi wa kisayansi na wenye maadili bora ya kujali wananchi kuanzia katika mikoa.

Alisema mambo aliyoyafanya katika kipindi chake cha uongozi mpaka sasa pamoja na kuwa ni mengi, lakini hataweza kuyamaliza kwani hata Mwalimu Julius Nyerere alitumikia Taifa kwa miaka 25 lakini hakuyamaliza.

Pia Ali Hassan Mwinyi alitumikia Taifa miaka 10 naye hakuyamaliza hali kadhalika Benjamin Mkapa pamoja na miaka 10, naye hakuyamaliza. habari kwa hisani ya www.habarileo.co.tz

No comments: