Jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa Tanzania limembana Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, kuhusu suala la mgombea binafsi. Majaji hao walimtaka Masaju awaeleze ni mahakama ipi yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
Masaju amesema, Katiba ni suala la Muungano; hivyo yenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo ni Mahakama Kuu ya Muungano na si ya Tanzania Bara, ambayo ilijipa jukumu ambalo si lake. Hoja hiyo iliwafanya majaji wamuulize maswali mengi wakitaka aoneshe mahali ilipo Mahakama Kuu ya Muungano yenye hadhi ya kusikiliza shauri hilo.
Lakini akiendelea kutetea hoja yake, Masaju aligeuka na kusema suala la Katiba ni la Muungano hivyo uamuzi wake si wa Mahakama bali ni lazima ufanywe na Bunge na uungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge kutoka Bara na Visiwani.
“Huu ndiyo utaratibu na si mahakama kukifuta au kukirekebisha kifungu cha Katiba,” alisema Masaju. Allisema kilichofanywa na Mahakama Kuu, ni kujitwisha jukumu la Bunge.
Amesema kama kuna upungufu kwenye Katiba, mlalamikaji hapaswi kwenda mahakamani, bali kwenye asasi zisizokuwa za Serikali au kumwambia mbunge wake aliwasilishe bungeni. Kesi hiyo inasikilizwa na majaji saba wa Mahakama ya Rufaa Tanzania; Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, Eusebio Munuo, Januari Msofe, Nathania Kimaro, Mbarouk Salim, Benard Luanda na Sauda Mjasiri. habari kwa hisani ya www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment